Kwa Simba, kesho Jumamosi huenda ikawa ndiyo mwisho wa msimu, hesabu ipo hivi...
Simba wanaweza kuumaliza msimu wao kesho au wakaamua kuuzika kabisa, au wakaamua kuendelea kupambana kwenye kazi ngumu zaidi.
Ndiyo, Simba kesho wanacheza mchezo wa nusu fainali wa Kombe la FA dhidi ya Azam FC, mchezo ambao kila mmoja anajua kuwa utakuwa mgumu na wenye heshima zaidi kwa Simba na Azam pia.
Pamoja na kwamba timu zote zinatafuta nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, lakini Simba wanaonekana kuwa na uchu mkali zaidi na ili watimize lengo lao la kukosa nafasi hiyo kwa miaka minne, basi wanatakiwa kuhakikisha wanapata ushindi kesho.
Kama Simba watashinda, basi watakuwa wakiishangilia Yanga Jumapili ili nayo ishinde wakutane wote kwenye fainali.
Hali itakuwa nzuri zaidi kwa vijana hao wa Msimbazi, kwani Yanga wakishinda ina maana kuwa tayari wawakilishi wawili wa michuano ya kimataifa kwa mwakani watakuwa wameshapatikana kwa kuwa kama Simba watatwaa ubingwa wa Ligi kuu bara na kutwaa ubingwa wa Kombe la FA basi atamuachia Yanga nafasi ya kombe la Shirikisho, lakini kama Simba nao watatoa ubingwa kwenye makombe yote watawaachia Yanga.
Hii inaonyesha kuwa ili timu hizo ziweze kupata tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa mwakani, basi lazima zote zishinde kwenye michezo yao ya kesho na keshokutwa.
Lakini hali itakuwa ngumu kwa Yanga kama Azam wataingia fainali, halafu wenyewe wakakosa ubingwa wa Tanzania Bara.
Endapo Azam wataingia kwenye fainali wakakutana na Yanga kwenye mchezo huo, na Yanga wakawa wameshatwaa ubingwa ubingwa wa Tanzania Bara, basi Azam atakuwa na uhakika wa kufuzu kwa michuano ya kimataifa, lakini kama ataingia na Yanga ambayo haina ubingwa, basi vita itakuwa kubwa sana kwani mshindi wa fainali ndiye atakayepanda ndege mwakani.
Hali hii inaonyesha kuwa kama Azam wakifuzu kwenye fainali basi watatakiwa kuwashangilia Yanga kwenye michezo yao yote iliyobaki ili timu hiyo ya Jangwani itwae ubingwa na wenyewe wawe nafasi ya kimataifa.
Kwa hiyo hakuna ubishi kuwa michezo hii miwili inaweza kuongeza kasi kwenye Ligi Kuu Bara au ikaimaliza kasi hiyo, kwa kuwa Simba 'tageti' yao ya kwanza ilikuwa michuano ya kimataifa tu.
Ni ukweli kwamba fainali ya Simba na Azam ni kesho, hilo halina ubishi atakayecheza karata yake vizuri basi atakuwa amejiweka kwenye asilimia 99 za kukwea pipa ndiyo maana yeyote atakayeshinda basi atashangilia sana.
Lakini pia Yanga nao wana hali hiyo hiyo, pamoja na kwamba wengi wanaona kuwa Yanga ana kazi ndogo kwa Mbao FC kwenye mchezo wake wa Jumapili lakini huu ni uongo.
Kama Yanga watakwenda na imani kuwa wana uhakika wa kushinda basi watajiweka kwenye hali ngumu, kuna uwezekano Mbao wakaiwakilisha nchi wakiwa wameshuka daraja.
Na ukweli ni kwamba wakienda fainali kwa kanuni zetu wakakutana na Simba ambao wameshatwaa ubingwa basi watapewa tiketi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa hiyo timu zote zinatakiwa kujua kuwa mechi hizi za wikiendi ndiyo zimeshikilia msimu wao wote.
Kwa Simba, kesho Jumamosi huenda ikawa ndiyo mwisho wa msimu, hesabu ipo hivi...
Reviewed by Steve
on
Friday, April 28, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment