Ngoma aamua kutimkia Sauzi kimya kimya, Meneja na Daktari wazungumza
Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma, ameendelea kuivuruga timu hiyo na safari hii imeelezwa ameondoka nchini na kuelekea Afrika Kusini bila ya kutoa taarifa kwa uongozi.
Ngoma, hivi karibuni aliingia kwenye mtafaruku na viongozi, pia mashabiki wa timu hiyo akidai ana majeraha huku taarifa zikiwepo yupo fiti na amegoma makusudi kucheza.
Mshambuliaji huyo, tayari amekosa michezo kadhaa ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na ile ya kimataifa kutokana na majeraha ya goti, nyonga.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, mshambuliaji huyo ameondoka nchini mwenyewe na kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kujitibu majeraha hayo.
Mtoa taarifa huyo alisema Ngoma akiwa nchini humo atatumia gharama zake kwa ajili ya kujitibia licha ya kuwepo makundi mbalimbali ya WhatsApp waliokuwa wakichangishana kwa ajili ya kumtibia yeye na beki raiwa wa Togo, Vincent Bossou.
"Tumepata taarifa za Ngoma kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kwenda kujitibia majeraha ya goti na nyonga iliyokuwa inamsababishia azikose baadhi ya mechi za michuano ya kimataifa, ligi kuu na Kombe la FA.
"Tumesikia anakwenda kujigharamia mwenyewe matibabu yake wakati uongozi na baadhi ya mashabiki walikuwa wanachangishana kwa ajili ya kufanikisha matibabu yake huko Sauzi, hivyo tumeshangazwa na mshambuliaji huyo," kilisema chanzo cha taarifa.
Alipotafutwa meneja mkuu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, kuzungumzia hilo, alisema:
"Hizo taarifa ninazisikia kama wewe ulivyosikia, sina taarifa rasmi juu ya taarifa hiyo."
Naye Daktari Mkuu wa Yanga, Edward Bavu alisema: "Sijapata taarifa rasmi za Ngoma kuondoka, nilizisikia taarifa hizo za kuondoka lakini hajanambia na kama ameondoka basi alitakiwa aniambie, ngoja nifuatilie halafu nitakupa taarifa rasmi."
Ngoma aamua kutimkia Sauzi kimya kimya, Meneja na Daktari wazungumza
Reviewed by Steve
on
Friday, April 28, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment