Propellerads

Kuhusu rufaa ya Simba kwa Kagera Sugar mambo yapo namna hii, Wambura afafanua




Zile pointi tatu walizozipata Kagera Sugar kutoka kwa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliopigwa Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba zimeanza kunukia kwa wekundu hao wa Msimbazi.

Katika mchezo huo Kagera waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku wakimchezesha beki wake, Mohamed Fakhi, ambaye Simba walimkatia rufaa wakidai alichezeshwa kimakosa kwani alikuwa na kadi tatu za njano.

Kufuatia hali hiyo, Simba waliwasilisha rufaa yao kwa Kamati ya saa 72, wakidai Kagera walikiuka taratibu na kanuni za Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara.

Wekundu hao wanamlalamikia Fakhi kuwa alionyeshwa kadi ya njano katika michezo mitatu mfululizo ambayo ni dhidi ya Mbeya City, uliopigwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Desema 17 mwaka jana, dhidi ya African Lyon, mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Kaitaba, Januari 18 mwaka huu.

Mchezo mwingine ni dhidi ya Majimaji, uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Machi 4, ambapo kisheria hakutakiwa kucheza mechi dhidi ya Simba jambo ambalo limewafanya Wekundu hao wa Msimbazi kumkatia rufaa mchezaji huyo.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ligi Kuu, Boniface Wambura, amefunguka kwamba Kamati ya saa 72 ilikutana juzi jioni na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo na suala hilo lakini kikao hicho kinatarajiwa kuendelea tena Alhamisi ijayo.

Alisema kikao hicho kimeshindwa kufikia mwafaka juu ya suala hilo kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya mambo hivyo kuazimia kuendelea tena Alhamisi na baadaye kutoa maamuzi.

"Kikao kilifanyika jana (juzi), lakini hakikumalizika hivyo kimepangwa kuendelea tena Alhamisi ambapo maamuzi yatakayofikiwa ndiyo yatatolewa taarifa kamili," alisema Wambura.

Chanzo:Dimba
Kuhusu rufaa ya Simba kwa Kagera Sugar mambo yapo namna hii, Wambura afafanua Kuhusu rufaa ya Simba kwa Kagera Sugar mambo yapo namna hii, Wambura afafanua Reviewed by Steve on Sunday, April 09, 2017 Rating: 5

No comments:

Propellerads
Powered by Blogger.