Hivi ndivyo maandalizi kwa ajili ya Waarabu yanaendelea Jangwani, vikao na mikakati lukuki
Yanga wameonyesha kwamba safari hii hawataki tena kuwa wateja wa Waarabu na wameanza mikakati yao kwa kufanya vikao usiku na mchana ili kuhakikisha wanawatoa MC Alger, kwenye mchezo wa marudiano wa kusaka nafasi ya kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Bao la Thaban Kamusoko lilitosha kuwapa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya MC Alger kwenye mchezo wa kwanza wa michuano hiyo uliofanyika Jumamosi ya wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa, sasa miamba hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakuwa na kazi nzito mjini Algiers nchini Algeria wakati wa mchezo wa marudiano utakaofanyika uwanja wa Omar Hamadi Jumamosi.
Hivyo klabu hiyo ya Jangwani itasafiri hadi Algeria kwenda kusaka ushindi au sare ya namna yoyote mbele ya Waarabu hao, huku wakijua kwamba watakumbana na vigingi ikiwamo figisu mbalimbali na ndio maana walianza vikao bab kubwa mara moja baada ya mechi ya kwanza.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji Yanga, amefunguka kuwa wamefanya vikao kadhaa ya kujadili mchezo huo wa marudiano pamoja na kupanga mikakati kabambe ya kuwang'oa Waarabu.
"Safari hii hatutaki kuendelea kuwa wateja wa Waarabu kila mara, kwani uwezo wa kuwatoa upo na ndio maana tumeamua kufanya vikao usiku na mchana ili kuweka mikakati mizito, ingawa siwezi kuanika kila kitu hadharani lakini mipango madhubuti ya kufanikisha lengo letu la kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya shirikisho imekamilika," alisema.
Hivi ndivyo maandalizi kwa ajili ya Waarabu yanaendelea Jangwani, vikao na mikakati lukuki
Reviewed by Steve
on
Tuesday, April 11, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment