Mjue nyota wa Yanga anayevuta mkwanja mrefu kuliko wote klabuni
TSH 6 Milioni: Mkwanja anaovuta
Haruna Niyonzima kwa mwezi
ACHANA na Azam ambayo ni klabu tajiri zaidi kwa sasa nchini, mabingwa mara 25 wa Ligi Kuu Bara Yanga, imeonyesha jeuri ya matumizi ya fedha na kuwaacha mbali watani wao wa jadi Simba ambao kwa sasa wanaonekana kuwa wa kawaida katika suala zima la mkwanja.
Taarifa za ndani zilizonaswa na Mwanaspoti zimebainisha kuwa Yanga inatumia Sh 120 milioni kwa mwezi kuwalipa mishahara wachezaji wake wote, benchi zima la ufundi na sekretarieti yake, fedha ambazo ni karibu mara mbili ya zile zinazotumiwa na watani wao wa jadi Simba.
Mwanaspoti ilienda mbali zaidi na kubaini kuwa wachezaji ambao wanachota mkwanja mkubwa katika mishahara pale Yanga ni pamoja na Haruna Niyonzima anayechukua dola 3000 (Sh 6 milioni) sambamba na Andrey Coutinho, Donald Ngoma na Vincent Bossou wanaochukua pia kiasi kama hicho cha fedha.
Mbali na nyota hao pia kuna wengine kadhaa kama akina Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko nao wanavuta mkwanja mrefu Jangwani pesa ambazo kwa baadhi ya nyota wa Simba na hata wa Yanga wenyewe wanazisikia tu redioni.
Wakati Jangwani wakitanua hivyo kifedha, watani zao ambao wanatarajiwa kukutana nao Septemba 26 kwenye mchezo wa duru la kwanza la msimu huu wa Ligi Kuu Bara inayoanza Jumamosi, taarifa kutoka Simba zinaeleza kuwa timu hiyo inatumia Sh 75 milioni pekee.
Fedha hizo kwa mwezi ni za kuwalipa wachezaji, benchi la ufundi la timu hiyo na sekretarieti yake.
Hata hivyo kutumika kwa fedha kiduchu Simba ni kutokana na uwezo mkubwa wa viongozi hao kufanya biashara na kuwabana watumishi wao, tofauti na ilivyo kwa watani zao Yanga ambao wakitajiwa kiasi chochote cha fedha huwa hawana cha kuuliza zaidi ya kukubali mara moja.
Wachezaji wanaochukua fedha nyingi katika malipo hayo pale Msimbazi ni Waganda Hamis Kiiza na Juuko Murshid wanaochukua dola 2000 (Sh 4 milioni) kila mwezi wakati wazawa Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude wakichukua Sh 2 milioni kwa mwezi.
Yanga imeipiga bao pia Simba katika malipo ya kocha ambapo kocha wao Mdachi Hans Van Pluijm anachukua dola 10,000 (Sh 20 milioni) kwa mwezi wakati kocha wa Simba, Dylan Kerr anachukua dola 6,000 (Sh 12 milioni kwa mwezi).
Kutokana na matumizi hayo inamaanisha kuwa Simba na Yanga zinalazimika kuchomoa fedha zao za mifukoni kujazia katika zile zinazotoka kwa wadhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Awali TBL ilikuwa ikitoa Sh 35 milioni kwa kila klabu lakini taarifa zinadai kuwa mikataba hiyo imeboreshwa kidogo lakini bado ni pungufu ya matumizi hayo.
Hii inamaanisha kwamba Yanga hulazimika kutoa zaidi ya Sh 70 milioni kila mwezi kujazia zile za TBL wakati Simba wao hutoa kati ya Sh 30-35 milioni pekee katika kuziba mabonde hayo.
CHANZO: GAZETI LA MWANASPOTI
Ungana nasi kupitia Facebook kwa ku like ukurasa wetu wa Kandanda 24 na tuffollow Twitter @Kandanda 24
Mjue nyota wa Yanga anayevuta mkwanja mrefu kuliko wote klabuni
Reviewed by Steve
on
Tuesday, September 08, 2015
Rating:
Reviewed by Steve
on
Tuesday, September 08, 2015
Rating:

No comments:
Post a Comment