Propellerads

Zesco kuwapa sapoti ya nguvu Yanga mbele ya Zanaco, mipango kedekede yasukwa

Zesco ya Zambia imeonekana kuamua 'kununua kesi'  inayowakabili Yanga dhidi ya wapinzani wao wa nchini kwao, Zanaco katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi jijini Lusaka.

Baada ya kupata sare ya bao 1-1 mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, Zanaco wanaonekana kuwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele kama alivyojinadi mmoja wa washambuliaji wao Mghana, Kwame Attram.

Lakini Zesco wanaonekana kutokuwa tayari kuona Zanaco wakiwatoa Yanga kutokana na sababu kubwa mbili.

Sababu ya kwanza ni upinzani uliopo baina ya timu hizo kiasi kwamba hakuna ambayo ingependa kuona mwenzake akifanikiwa, hasa katika anga ya kimataifa.

Ukiachana na hiyo, pili ni kitendo cha kikosi cha Yanga kuundwa na kiungo wao wa zamani Justice Zulu pamoja na aliyekua kocha wao, George Lwandamina.

Kiungo wa Zesco, Mishack Chaila amethibitisha kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha Yanga wanaitoa Zanaco.

"Yanga wakitulia wanashinda hiyo mechi, Lwandamina ni kocha mzuri tunamfahamu sana, ni mzuri katika mbinu, nina imani ushindi watapata. Huku Zesco kila mmoja anataka Yanga ishinde na kusonga mbele," alisema Chaila.

Kwa upande wake, mtoto wa Lwandamina anayefahamika kwa jina la Junior, alisema familia, marafiki, jamaa zao, mashabiki wote wa Zesco pamoja na Watanzania wanaoishi Zambia, wamepanga kuipa Yanga mapokezi ya aina yake pamoja na kuwafichulia mbinu zote zitakazowezesha kuiua Zanaco.

"Mchezo utakuwa mgumu 50/50, lakini Yanga watakuwa na faida moja ya kupata sapoti ya kushangiliwa kutoka kwa mashabiki wa Zesco na Watanzania wengine wanaoishi huku ambao wamepanga kufanya kila linalowezekana ili Zanaco watolewe," alisema.


Zesco kuwapa sapoti ya nguvu Yanga mbele ya Zanaco, mipango kedekede yasukwa Zesco kuwapa sapoti ya nguvu Yanga mbele ya Zanaco, mipango kedekede yasukwa Reviewed by Steve on Tuesday, March 14, 2017 Rating: 5

No comments:

Propellerads
Powered by Blogger.