Unaambiwa huu ndio ujanja walioufanya Yanga kwa Simba, ni noma basi!!
UKISIKIA umafia basi ndio huu. Inafahamika wazi kuwa Simba na
Yanga zinatarajiwa kuvaana kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2015-2016 Septemba 26 katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Pambano hilo litachezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam wakati timu zote zikiwa zimeshacheza mechi tatu kila moja.
Lakini katika kuhakikisha kuwa wanaifanyia udukuzi mapema watani zao na kuwadhibiti kimbinu, mabingwa watetezi Yanga waliamua kuwatangulia wenzao hatua moja mbele baada ya kuvuka bahari kimya kimya hadi visiwani Zanzibar kuwasoma bila wenyewe Msimbazi kufahamu lolote.
Unajua ilikuwaje? Simba baada ya kuvunja kambi yao ya visiwani humo kwa muda ili kurejea jijini Dar es Salaam kufurahia tamasha lao la Simba Day, iliamua kukaa kwa muda kabla ya kurejea tena Zanzibar kujiandaa na msimu mpya wa ligi itakayaoanza Jumamosi.
Tayari ilikuwa inafahamu itaanza kibarua chao Uwanja wa Mkwakwani, Tanga dhidi ya African Sports waliorejea katika Ligi Kuu msimu huu, ikiwa ni baada ya miaka zaidi ya 20 tangu ishuke daraja mwaka 1991.
Watani zao, yaani Yanga wakaona isiwe tabu kwa kuamua kuwawahi mapema kwa kumtuma Katibu Mkuu wao, Dk Jonas Tiboroha ambaye kitaaluma ni kocha ili kuifanyia Simba ushushushu wa kuisoma mbinu zake kisha akarejea kimyakimya jijini Dar es Salaam ili kutoa tathmini.
Tathmini ambazo zimeanza kufanyiwa kazi na benchi la ufundi katika kuhakikisha msimu huu Mnyama hachamoki mbele ya vijana wa Jangwani siku watakayokutana.
Mwanaspoti inadokeza kuwa umafia huo ulifanywa kwa siri kubwa bila kuwashutua upande wa pili na Tiboroha aliposakwa kuulizwa kisa cha kwenda Unguja kimya kimya, kwanza alishtuka na baadaye kutamka kwa kujiamini akisema: “Safari hii watatujua, tutakapokutana nao”.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tiboroha alisema katika safari yake hiyo ambayo haikuwa na lengo moja la kwenda kuwasoma Simba bali alikuwa na mambo yake binafsi, lakini amegundua kwamba kwa sasa Simba ni watani wao wa jadi, ila wapinzani wao kisoka kwa sasa ni Azam kulingana na utofauti aliougundua.
Alisema kwa sasa hawatatoa tathimini yote katika kuwasoma watani wao hao ambapo katika safari yake hiyo Tiboroha alifanikiwa kuwasoma Wekundu hao wa Msimbazi walipokuwa wakiumana na kikosi cha KVZ ambao walitoshana nguvu kwa kutoka sare isiyokuwa na mabao.
“Nimeona usajili wao watu walikuwa wanatuambia kwamba wana safu nzuri ya kiungo, mengi nimejionea mwenyewe nataka tu nikwambie kwamba hata Azam walikuwa wanatutisha kwamba wanakiungo imara, lakini tulipokutana nao mara ya pili kila kitu kilionekana pale huo ni uwezo wa makocha wetu katika kujua mbinu,” alisema Tiboroha.
“Hatutaki kuongea sana kwa sasa tupo katika hatua za mwisho kukamilisha michakato ya kuanza kwa ligi, tumekutana na viongozi wetu wa matawi tumejipanga na sasa tunamalizia mambo, ila hao Simba unaoniulizia acha tukutane nao Septemba 26 utapata jibu.
Ungana nasi kupitia Facebook kwa ku like ukurasa wetu wa Kandanda 24 na tuffollow Twitter @Kandanda 24
Unaambiwa huu ndio ujanja walioufanya Yanga kwa Simba, ni noma basi!!
Reviewed by Steve
on
Wednesday, September 09, 2015
Rating:
Reviewed by Steve
on
Wednesday, September 09, 2015
Rating:

No comments:
Post a Comment