Baada ya muda mrefu huenda hii ikawa ni dawa ya ushindi wa Simba Mkwakwani
KWA misimu mitatu sasa Simba haijaonja ushindi wowote kwenye Uwanja wa
Mkwakwani katika mechi za Ligi Kuu Bara. Na msimu huu inatarajiwa kuanza mechi zake ugenini kwenye Uwanja huo uliopo jijini Tanga kwa kuvaana na African Sports iliyorejea Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu iliposhuka daraja mwaka 1991.
Huenda ni miaka mingi mno tangu Wana Kimanumanu waionje Ligi Kuu, lakini bado mzimu wa kushindwa kupata ushindi jijini Tanga unaendelea kuisumbua Simba na safari hii, imepanga kutinga jijini humo kimafia kwa kuhakikisha inakata mzizi wa fitina.
Ni hivi, Msimbazi baada ya kujiuliza kwa muda mrefu juu ya kuchemsha kwao Mkwakwani, safari hii wameipata dawa yake. Ikiwa inajiandaa kuelekea huko kesho Alhamisi, Simba imeamua kuikabidhi timu hiyo kwa jopo la wazee likiongozwa na Omari Mtika, Hassan Dalali na Chuma Suleiman maarufu kwa jina la Bi Hindu.
Habari za ndani ya klabu ya Simba zinasema kuwa, viongozi waliamua kukutana na baadhi ya viongozi wa matawi kupanga mikakati ya kuhakikisha wanapata ushindi kwa mara ya kwanza kwa kuifunga African Sports.
Kikao hicho cha kuiua Sports iliyopanda daraja msimu huu ambao nao imepania kucheza kufa au kupona kuhakikisha wanailaza Simba kwenye uwanja huo siku ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, Septemba 12 kiliendeshwa na Rais wa Simba, Evans Aveva.
Mbali ya Aveva, wengine walioshiriki kikao hicho kilichofanyika Jumapili kwenye Ukumbi wa Sigara (TCC) Chang’ombe, ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Usajili, Idd Kajuna, Amina Poyo, Haruna Nazi kutoka Temeke, Yahya Athuman wa Ilala, Karim Boimanda ambaye ni Mwenyekiti wa tawi la Simba Damu Funs (SDF) na Ally Bane.
Habari hizo zimedokeza kuwa Baraza la Wazee linaloongozwa na Mzee Mtika, Dalali na Bi Hindu ndiyo waliopewa jukumu la kuongoza timu kwenye mechi hizo za ufunguzi za jijini Tanga ambapo baada ya kukwaruzana na Sports siku ya Jumamosi katikati ya wiki itaivaa Mgambo JKT.
“Ni mechi ngumu ndiyo maana tunaweka mikakati ya kuhakikisha tunashinda, tumekutana baadhi lakini baadaye tunaweza kuwaongeza wengine,” kilisema chanzo chetu.
Tangu mwaka 2012, Simba haijashinda Mkwakwani, katika mechi mwisho msimu wa 2012-2013 ambao ilitwaa taji lao la mwisho la Ligi Kuu, ilitoka 0-0 na Coastal Union, msimu uliofuata ilikuwa hivyo hivyo mbele ya Coastal kabla ya kulala 1-0 kwa Mgambo na msimu uliopita Simba ililazimishwa tena sare isiyo na bao na Coastal Union kabla ya kulala mabao 2-0 mbele ya maafande wa Mgambo JKT.
Ungana nasi kupitia Facebook kwa ku like ukurasa wetu wa Kandanda 24 na tuffollow Twitter @Kandanda 24
Baada ya muda mrefu huenda hii ikawa ni dawa ya ushindi wa Simba Mkwakwani
Reviewed by Steve
on
Wednesday, September 09, 2015
Rating:
Reviewed by Steve
on
Wednesday, September 09, 2015
Rating:

No comments:
Post a Comment