Rage awawakia Yanga: "Pilipili usioila yakuwashia nini?!"
Wakati Simba ikitarajia kujua hatima yao dhidi ya beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi, waliyemkatia rufaa kwenye kamati ya saa 72, Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo ya Msimbazi, Ismail Aden Rage, ameishukia Yanga kwa kuwaambia 'pilipip ya shamba inawashia nini'.
Kauli hiyo ya Rage inakuja siku moja baada ya Yanga kutangaza kwamba watakwenda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kuchunguza taarifa za waamuzi na makamisaa kuhusu rufaa hiyo ya Simba.
Lakini Rage akizungumza jana, aliijia juu Yanga na kusema inapaswa kuiacha kamati hiyo ifanye kazi yake ipasavyo kwani waliopaswa kulalamika ni Kagera Sugar na si wao.
"Hivi pilipili usioila inakuwashia nini? Yanga inawahusu nini? Yule mwamuzi ni wa Simba na Kagera. Sasa kinachowasumbua Yanga sijui ni kitu gani, wanapaswa kuacha kamati itimize majukumu yake," alisema Rage.
"Takukuru, TCRA unaweza kwenda kwa kuwa haki ya kisheria inakuruhusu, ila utakapothubutu kwenda mahakamani ujiandae kushushwa daraja," alisema.
Alimaliza kwa kuwataka Yanga kukaa pembeni msimu huu kwa kuwa miaka mitatu waliokuwa wakipokezana na Azam hawajaweza kufanya lolote la maana kwenye michuano ya kimataifa.
"Yanga wawaache wanaume (Simba) wafanye mambo yao msimu huu wakapeperushe vema bendera ya Taifa, yaani miaka yote mitatu waliokuwa wakishiriki wamekuwa wakipanda ndege mara moja na kurudi wawaache Simba na rekodi zao za kimataifa," aliongeza.
Simba kwa sasa wapo kileleni kwa pointi 58, huku mahasimu wao Yanga wakifuatia nafasi ya pili wakiwa na pointi 56, huku wakiwa na kiporo cha mechi moja mkononi. Kama Simba watashinda rufaa hiyo na kupewa pointi tatu na mabao mawili kama taratibu zinavyosema, basi kikosi hicho cha Msimbazi kitakuwa na jumla ya pointi 61 na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza tangu 2012.
Rage awawakia Yanga: "Pilipili usioila yakuwashia nini?!"
Reviewed by Steve
on
Thursday, April 13, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment