Mayanja aweka wazi matumaini ya ubingwa kwa Simba msimu huu, hesabu ipo hivi
Licha ya Simba kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, Wekundu hao wa Msimbazi wamesema bado hawana uhakika wa kuchukua ubingwa mpaka wapinzani wao wa jadi, Yanga watakapoteleza.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, mpaka sasa Simba inaongoza ikiwa na pointi 62 ikibakiwa na michezo mitatu kabla ya kumaliza msimu, huku ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56 na michezo mitano mkononi.
Endapo Simba ikishinda mechi zake zote tatu zilizosalia, basi itafikisha pointi 71, huku wenzao Yanga nao wakishinda mechi zao zote tano watafikisha idadi hiyo ya pointi ambapo bingwa atakuja kuamuliwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mpaka sasa Yanga imefunga mabao 50 na kufungwa 11, huku Simba ikifunga 46 na kufungwa 12.
Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanjaa, raia wa Uganda amesema kuwa kwa sasa ubingwa upo wazi baina ya timu hizo mbili, lakini wao wanaweza kuwa mabingwa endapo Yanga itateleza kwenye mchezo wake mmoja kati ya hiyo mitano.
"Bado mbio za ubingwa zipo wazi kati yetu na Yanga, kwa sasa tunaongoza ligi kwa tofauti ya pointi sita, lakini wapinzani wetu tumewapita michezo miwili, kama wakishinda watatufikia.
"Lakini bado tunaweza kuwa mabingwa wa msimu huu endapo Yanga watateleza kwenye michezo yao iliyosalia na sisi tukashinda yote kwa sababu michezo yetu yote iliyobaki tunacheza Dar ambapo tumekuwa na matokeo mazuri sana msimu huu," alisema Mayanja.
Katika michezo hiyo mitano, Yanga imebakiza mchezo mmoja tu wa ugenini dhidi ya Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na utachezwa siku ya mwisho wa msimu.
Mayanja aweka wazi matumaini ya ubingwa kwa Simba msimu huu, hesabu ipo hivi
Reviewed by Steve
on
Monday, April 17, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment