Hans Poppe afungukia tuhuma za Simba kutumia rushwa kupata ushindi
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ameibuka na kudai kwamba wapinzani wao wanaowatuhumu kwamba wanatoa rushwa wanakosea kutokana na wao kutumia fedha kwa wachezaji wao kwa ajili ya kuongeza morali ya kusaka ushindi.
Hivi karibuni Simba walituhumiwa kutoa rushwa kwa ajili ya kuwarubuni wachezaji kwa Mbao FC baada ya kutoka nyuma ya mabao 2-0 na kushinda kwa mabao 3-2 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza.
Kutokana na tuhuma, viongozi wa Mbao kupitia mwenyekiti wake, Solly Njoshi walimsimamisha kipa wao, Eric Ngwengwe ambaye alidaka kwenye pambano hilo.
Hans Poppe amesema anashangazwa na maneno hayo kutokana na kutokuwa na ukweli wowote ila inatokana na wapinzani wao kuchukia aina ya matokeo ambayo wamekuwa wakipata hasa kwenye mchezo huo wa Mbao.
"Tunashangazwa na maneno ambayo wanayasema wapinzani wetu kwamba tunatoa rushwa kwenye mechi zetu ili tupate ushindi zaidi kwenye ule mchezo wa Mbao ambao tulitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
"Kwanza nataka kuwaambia tutoe rushwa ili iweje maana mechi zote zinachezwa uwanjani, sasa hayo mambo ya rushwa yanaibuka kutoka wapi, na je wana ushahidi juu ya ambaco wanakisema?
"Sisi msimu huu fedha zetu tumeziwekeza kwa wachezaji kwa kuwapa fungu la kutosha katika kila mechi kuhakikisha kwamba wanaibuka na ushindi na hakuna jambo lingine kama wao wanavyodai na kusema," alisema Hans Poppe.
Hans Poppe afungukia tuhuma za Simba kutumia rushwa kupata ushindi
Reviewed by Steve
on
Wednesday, April 19, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment