Simba wamtaja kigogo wa TFF anayewakwamisha suala la mkataba wa Mbaraka Yusuph
Kitendo cha mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuph kufunga bao 'murua' katika mchezo dhidi ya Simba na kuchagiza ushindi kwa timu yake wa mabao 2-1, kumeongeza hasira kwa Wanamsimbazi ambapo sasa kuna jipya limeibuka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ameona isiwe tabu, amefungukia sakata la mchezaji huyo na kuamua kumtaja Rais wa Shairikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Wakati Simba wakidai huyo ni mchezaji wao, upande wa Kagera nao wamekuwa wakieleza kuwa huyo ni mchezaji wao na hachezi kwa mkopo bali wana mkataba naye rasmi usio wa mkopo.
Hans Poppe amesema kuwa hadi sasa hawana cha kufanya juu ya mchezaji huyo kwa kuwa tayari walishafika hadi ngazi za juu za TFF katika mamlaka inayohusika lakini sakata hilo halijapatiwa ufumbuzi.
Amedai labda kwa kuwa Rais wa TFF anatokea Kagera na mchezaji huyo kuwa wa Klabu ya Kagera inaweza kuwa sababu ya maamuzi ya mchezaji huyo kutochukuliwa maamuzi na kusababisha kudhurumiwa kwa haki yao.
"Kwa upande wetu kwa sasa hatuna hatua yoyote ile ya kuweza kuichukua kwa kuwa suala hilo lilishafika hadi ngazi za juu za TFF lakini hawakulitolea maamuzi hadi sasa hatuna cha kufanya, nadhani kwa kuwa mchezaji huyo ni wa Kagera na Malinzi ni wa Kagera ndiyo maana imekuwa hivyo.
"Sisi tulimtoa kwa mkopo lakini tulishangaa akipewa mkataba na Kagera, wao (Kagera Sugar) wana hati ya kumtumia kama mchezaji wao na sisi pia tuna leseni yake.
"Kama unakumbuka kuna kipindi Mbao FC nao walimkatia rufaa na sisi tulipeleka uthibitisho lakini hakuna kilichoamuliwa hadi sasa na jambo hilo bado lipo tu TFF.
"Kilichotokea ni hivi, sisi tulipeleka jina la Yusufu Mbaraka na wao (Kagera Sugar) wakabadili jina na kupeleka jina la Mbaraka Yusuph jambo ambalo si sahihi, tunachotaka sisi ni kuona wanatupatia barua kuwa mchezaji huyo acheze kwa mkopo Kagera kama ilivyo mwanzo na si kwa mkataba kama ilivyo sasa kwa kuwa sisi bado tunamtambua ni mchezaji wetu," alisema Hans Poppe.
Chanzo: Championi
Simba wamtaja kigogo wa TFF anayewakwamisha suala la mkataba wa Mbaraka Yusuph
Reviewed by Steve
on
Friday, April 07, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment