Ijue sababu ya Mkude na Ajibu kukalishwa benchi kwenye mchezo dhidi ya Mbao FC
Jumatatu iliyopita kikosi cha Simba kilicheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Hata hivyo katika mchezo huo, wachezaji wa Simba, Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu walipigwa benchi na nafasi zao kuchukuliwa na wachezaji wengine.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuanza kuhoji kutokana na kutowaona wachezaji hao uwanjani wakati timu yao ikionekana kuzidiwa maarifa na Mbao FC, hususan kipindi cha kwanza cha mchezo huo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai wachezaji hao hawakupangwa katika mechi hiyo kutokana na kutuhumiwa na uongozi wao kucheza chini ya kiwango dhidi ya Kagera Sugar, hata hivyo, Jumatano iliyopita wamepigwa mkwara mzito na kuonywa kuachana na tabia hiyo.
"Mkude na Ajibu walikuwa na matatizo na uongozi ndiyo maana katika mechi yetu na Mbao hawakupata nafasi ya kucheza lakini hivi sasa wamemalizana baada ya kuwekwa kiti moto.
"Uongozi ulikuwa ukiwatuhumu kucheza chini ya kiwango katika mechi yetu na Kagera Sugar ambayo tulifungwa kwa mabao 2-1, hivyo ukalitaka benchi la ufundi kutowatumia dhidi ya Mbao ndiyo maana siku hiyo hawakuweza kucheza," kilisema chanzo hicho cha habari.
Walipotafutwa wachezaji hao hawakupatikana kwa kuwa walikuwa katika maandalizi, pia alipoulizwa kuhusiana na hilo kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja hakutaka kuzungumza chochote.
Ijue sababu ya Mkude na Ajibu kukalishwa benchi kwenye mchezo dhidi ya Mbao FC
Reviewed by Steve
on
Friday, April 14, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment