Maneno ya Rio Ferdinand baada ya kustaafu soka.
Beki wa zamani wa Manchester United na
timu ya taifa ya Uingereza Rio Ferdinand ametangaza rasmi kutundiga
daluga kusakata kabumbu. Rio aliachwa na QPR baada ya klabu hiyo
kuteremka daraja msimu huu.
QPR imewaacha Joey Barton, Rio Ferdinand
na Bobby Zamora. Ferdinand ambaye ni nahodha wa zamani wa Uingereza kwa
sasa ameamua rasmi kuachana na mchezo wa soka na kuanza maisha mapya
uraiani na biashara nyingine. Rio ameiambia amesema hivi “Baada
ya miaka 18 ya kusakata kabumbu kama mchezaji wa kulipwa, sasa nimeona
ni muda muafaka kwangu kustaafu mchezo huu ninaoupenda zaidi.”
“Nikiwa kama mtoto wa miaka
12, niliweza kupiga mpira kule Friary Estate ambayo ipo Peckham,
sikuwahi kuwa na ndoto ya kuichezea timu ya West Ham timu ambayo ndio
nilianzia maisha pale. Nimewahi kuwa nahodha wa Leeds United, nimeshinda
kombe la klabu bingwa Ulaya nikiwa na Manchester United na kuungana kwa
mara nyingine tena na kocha wangu wa kwanza Harry Redknapp hapa Queens
Park Rangers.”
“Siku zote nitaheshimu
michezo 81 ambayo nimejumuika na timu ya taifa ya Uingereza, nikijivunia
sana fahari hiyo. Hizi zote ni kumbukumbu ambazo kamwe hazitosahaulika
katika maisha yangu.Ukianza taaluma yoyote ile kila kijana anahitaji mtu
wa karibu wa kumshauri. Nilijikuta niko mikononi mwa Dave Goodwin,
Meneja wa wilaya huko Blackheath na Tony Carr meneja wa timu ya vijana
ya West Ham. Walinipa mafunzo mema ambayo yamedumu kwa takribani kipindi
chote nilichokuwa katika mchezo wa soka. Nitaendelea kuwaheshimu
daima.”
“Ningependa kutoa shukrani
zangu za dhati kwa Chris Ramsey, Harry Redknapp, David O’Leary na David
Moyes ambao waliniwezesha katika nyakati tofauti katika maisha yangu ya
soka bila ya kusahau wafanyakazi wengine katika timu ambao walionyesha
kunijali kwa miaka yote. Pia wachezaji wote ambao nimewahi kucheza nao.
Ningependa kutoa shukrani kwa timu iliyonisaidia wakati nikiwa nje ya
mchezo huu, Jamie Moralee na kila mtu katika kipindi hiki kipya
ninachokianza rasmi.”
“Kushinda makombe kwa kipindi
cha miaka 13 nikiwa na klabu ya Manchester United ilinifanya nifanikiwe
kila kitu nilichokuwa nikikitamani katika tasnia ya soka. Tangu utotoni
mpaka wakati huu, hicho ndicho nilichokuwa nikikiwaza mara zote. Vyote
hivyo sidhani kama vingewezekana bila ya kiungo muhimu kabisa ambaye
ni, Sir Alex Ferguson. Upeo wake mkubwa katika macho yangu utaendelea
kudumu daima. Kwa mtazamo wangu yeye ndiye atabaki kuwa kocha bora
kabisa katika historia ya mpira wa Uingereza.”
“Pia ningependa kutoa
shukrani zangu za dhati kwa mke wangu Rebecca na familia yangu, akiwemo
mama na baba yangu kwa kujitolea maisha yote juu yangu pia faraja na
ushauri wao waliokuwa wakinipa kwa kipindi chote nilichokuwa nikisakata
soka”
“Na mwisho kabisa, ningependa
kuwashukuru mashabiki wote katika klabu zote kwani bila yao mpira huu
uliojaa utaalamu wa hali juu usingekuwepo. Nitamkumbuka kila mmoja wenu
kwenye jioni hii ya siku ya Jumamosi.”
Maneno ya Rio Ferdinand baada ya kustaafu soka.
Reviewed by Steve
on
Sunday, May 31, 2015
Rating:
Reviewed by Steve
on
Sunday, May 31, 2015
Rating:
